MPANGO SHIRIKISHI WA KUPANUA KILIMO CHA KOROSHO UTAONGEZA MAPATO KWA MKULIMA NA TAIFA:
Na Godwin Msalichuma,
Mtwara,
NI MUDA mrefu Tanzania imekuwa ikisema kuwa kilimo ni uti wa mgongo wa taifa letu kwakuwa asilimia kubwa ya wananchi wanajishughulisha na ukulima wa mazao mbalimbali ya chakula na biashara, na katika kujihusisha na uzalishaji wa biashara huwa pia kunaingizia taifa pesa za kigeni kwa kuyauza nje ya nchi yetu.
Leo nataka tuangalie zao kubwa hapa nchini linalolimwa ukanda wa pwani na kusini ya nchi yetu ya Tanzania,inasemekana mti huu wa korosho uliletwa hapa kwetu kuanzia miaka ya 1880 au zaidi iliyopita na waliouleta ni wakoloni wa kireno waliutoa America ya kati na kusini hususani nchini Brazili na kuanza kulimwa mwambao mwa pwani yaani Tanga, Lindi na Mtwara.
Na baada ya vita kuu ya pili ya Dunia hapa nchini zao hili lilianza kupata umaarufu sana kwani India iliweza kununua tani 7,000 za korosho ghafi, na kwa kipindi cha miaka kumi na tano hadi kufikia mwaka 1960 uzalishaji wa korosho hapa nchini uliongezeka mara sita hadi kufikia tani 42,000 za korosho ghafi zilizouzwa nje ya nchi.
Kazi kubwa ya upandaji mikorosho nchini ilifanyika miaka ya sitini, kabla na baada ya uhuru, aidha ari kwa wakulima kupanda mikorosho mipya iliamshwa na kauli mbiu ya serikali mara baada ya uhuru ambayo ilisisitiza maisha bora shambani, uzalishaji wa korosho ulipanda na kufika kilele mwaka 1974 zilipozalishwa tani 145,000 na rekodi hii haijawahi kufikiwa tena hadi leo.
Baada ya hapo uzalishaji wa korosho ulianza kupungua mwaka hadi mwaka na kufikia kiwango cha chini kabisa cha tani 16,552 msimu wa mwaka 1986/1987, serikali ikaingilia kati na kutafuta wadau wa maendeleo ili kulifufua zao hili ambapo msimu wa mwaka 1990/1996 mapato yakaongezeka na kufikia tani 95,000 na misimu iliyoendele ya 2000/2001 korosho ilifikia kilele tani 122,283 ambazo katika miaka ya hivi karibuni imekuwa ndoto kuzifikia tena rekodi hizo.
Tumeshuhudia tena baada ya hapo zao likaanza kuporomoka tena kwa kasi sana na msimu wa mwaka 2001/2002 uzalishaji ulifikia tani 67,369,kuna sababu nyingi tu za kuporomoka kwa zao la korosho nchini ambazo ziko ndani ya uwezo wetu kuzikabili, kubwa tu ni kujipanga vizuri kila mmoja kwa nafasi yake na kuweza kufikia nafasi ya juu Duniani kwa uzalishaji na uuzaji wa korosho.
Bodi ya korosho ambayo ndiye yenye dhamana na zao hili iliamua kuja na mkakati shirikishi ambao utasaidia kufufua na kupandisha uzalishaji wa korosho nchini pamoja na kuhimiza ubanguaji ili kuongeza thamani ya zao hili kabla ya kuuza nchi za nje na kuinua kipato kwa mkulima na taifa zima, mkakati huo ulishaanza tangu mwaka 2003 na utaishia mwaka 2013 ndipo watakapo kaa chini na kutathimini kilichopatikana katika mpango huo.
Hatua ya kwanza katika mkakati shirikishi huo umeona kuwa wadau wengi wa zao hili hapa nchini ni wakulima wadogo wadogo kwahiyo wataanza kwa kupanda mikorosho mipya, kukarabati ya zamani na kuboresha utunzaji wa mashamba ya korosho yaliyopo na walengwa ni wakulima wadogo.Nadhani mkakati huu unaweza kuleta maana haswa katika kipindi serikali inapokuja na kauli mbiu ya kilimo kwanza na mapinduzi ya kijani,la msingi ni kuzingatia sera itakayo tumika ili kuunda mpango kazi ambao utaendena na hali halisi ya wakati huu.
Kwa kuwa wakulima wengi ni wadogo wadogo hapa nchini, serikali inaombwa kushuka kabisa mpaka kuwafikia hawa maana wengi wanaishi vijijini,miundombinu ilekebishwe ili waweze kupata mbegu/miche, madawa na pembejeo katika misimu ya uzalishaji wa korosho, na pia waunda sera wawasikilize wakulima wanasema nini kuhusu matatizo yanayojitokeza katika uzalishaji ili sera hizo ziendane na wakati.
Haya pia yalithibitishwa na Mkurugenzi wa kilimo na ubanguaji Bw.Luseshelo Silomba kutoka bodi ya korosha Tanzania Mtwara akiwa ofisini kwake wakati wa mahojiano na mwandishi wa habari hizi na haya ndiyo aliyoyasema.
“ Tumejipanga vizuri katika mpango huu kuona kuwa tunaondoa kero za wananchi katika zao hili la korosho…kwani kwa muda mrefu malumbano kati ya serikali na wananchi yamekuwa makubwa …..wengi mtakumbuka mpaka tumeweza kuhojiwa na vituo vya Television kuonyesha kuwa suala hili linawakera wanachi….kwahiyo serikali imekuja na mpango huu kuona kero zinapungua au zinakwisha kabisa nah ii ni njia ya kutatua kero za wananchi katika maeneo yao”alisema Bw.Silomba
Mkakati huu pia unashirikisha wadau katika kutekeleza majukumu yake kama vile vituo vya utafiti wa mbegu bora na uzalishaji wa miche ili kuwapatia wakulima waweze kuzalisha kwa ubora unaotakiwa,maafisa kilimo na wagani nao wasiachwe mbali kwani kwa kufanya hivi kituo cha utafiti Naliendele Mtwara kimeanza kutoa tena mafunzo ya watalaamu wa kilimo na ugani ambao watashirikiana na wakulima katika kufufua na kuendeleza tena zao hili lenye umaarufu Duniani.
Bodi ya korosho yenyewe ni msimamizi wa mpango huo na ni kitovu cha sekta ya korosho hapa nchini kwani kwayo imepewa jukumu la kuelimisha jamii pamoja na kuishauri serikali na vyombo vyake kama vile wakuu wa mikoa, Halmashauri za wilaya zinazolima korosho,vyama vikuu vya ushirika,vyama vya ushirika vya msingi, vyama vya wakulima,wafadhili na asasi mbalimbali hapa nchini pamoja na sekta binafsi kwani kutoka katika sekta hii tunaweza kupata wakulima wakati na wakubwa ambao wataongeza uzalishaji na kutoa ajira vijijini ili kupunguza umasikini katika jamii yetu.
Kwani sekta binafsi inauwezo pia wa kukopesheka na mabenki na kuzalisha zaidi na wanaweza kuweka viwanda vya kubangua korosho hizo kabla ya kuziuza nje ya nchi, kwahiyo hapa kunauwezekano mkubwa wa kuzaliwa ajira nyingi za mashambani na viwandani na ni mwanzo wa mapinduzi ya viwanda,mapinduzi ya viwanda huanzia na viwanda vidogo vidogo mpaka kupata viwanda vikubwa.
Na tukianza kuongezea thamani mazao yetu ndio mwanzo wa kuanzisha ajira zetu na kuongeza pato la wakulima na pato la nchi kuingiza pesa za kigeni,nchi nyingi zilizoendelea kiviwanda zilianza na viwanda vidogo vidogo vya usindikaji mpaka kufikia viwanda vikubwa vinavyounda zana za kilimo mfano ni Wakorea, kazi kubwa mnayo bodi ya korosho Tanzania.
Na lililokubwa kushinda yote ni kuona mpango mkakati huo unatekelezwa na unafanikiwa lakini hauwezi kufanikiwa kama wadau wote hawatafanya kazi kama timu,tusije tukafika mwisho tunaanza kutafuta mchawi ni nani wakati wengine hawataki kushirikiana ili kilimo kwanza kilete maana na kuyafikia mapinduzi ya kijani ya kweli na kuyakamata malengo ya milenia.
Mwisho
0713 609255
0787 609255
Email:msalichumag@gmail.com
www.msalichuma.blogspot.com
Korosho kutoka kwa mkulima Mtwara, kama serikali ikimwezesha mkulima vizuri umasikini utapungua miongoni mwa wananchi.Picha na Godwin Msalichuma.
Korosho zilizobanguliwa kabla ya kukaangwa na kufungashwa. Picha na Godwin Msalichuma.
Korosho ambazo tayari zimesha fungashwa na Mjasiriamali mdogo kutoka Mtwara God’s entrepreneur Ltd, email: msalichumag@gmail.com
No comments:
Post a Comment
Any