Na Godwin Msalichuma,
Mtwara,
UKILIONA shina lake
unaweza ukashangaa sana kwani kwa mbali unaonekani kama mmea mmoja hatari na
haramu, mara ya kwanza nilijiuliza nilipokutana na shamba kubwa la maonyesho kwa
wakulima ambalo lipo katika kituo cha utafiti wa kilimo na mifugo cha
Naliendele Mtwara kilichopo kama kilometa 15 kutoka mjini.
Kilichonishangaza katika mmea huo ni kwamba kuona kuwa
unafanana kwa mwonekano haswa ukiwa mbali kidogo kama mimi nilivyokuwa ndani ya
gari nikaona kama bangi ikanishangaza pia kulimwa tena karibu na barabara
iendayo Tandahimba hadi Newala karibu kabisa na kituo hicho kikubwa cha utafiti
katika Afrika.
Kabla sijauliza nilijiuliza mwenyewe moyoni kuwa ina
maana kuwa katika kituo hiki cha utafiti wa kilimo wanatafiti pia zao la bangi?
nikasema hapana itanibidi niulize wenyeji nilionao katika gari hili ninayoyaona
ni kweli au naota ndoto za mchana.
Lakini kuna usemi unaosema kuwa anayeuliza anataka
kujifunza ukanipa matumaini ya kuuliza ndipo nilipochukua uamuzi wa kufanya
hivyo, nikamgusa jirani yangu tuliyekaa naye kiti kimoja “samahani kaka huku
kwenu bangi zinaruhusiwa kulimwa”? Yule bwana alishituka kidogo na kunijibu
kuwa hapana haziruhusiwi!.
Nikamwuliza tena kuwa sasa zile ninazoziona pale
siyo bangi au macho yangu mabovu? Alicheka kidogo kabla hajanijibu kwa mara ya
pili na kusababisha abiria wengine katika gari lile kukaa kimya na kutugeukia.Nadhani
wengi huenda walisikia swali langu na wakataka kujua kuwa yule niliyemwuliza
atajibu nini na pengine wengine wakafikiria huenda mimi siyo Mtanzania ndiyo
maana nauliza swali kama lile.
Lakini bwana yule hakusita ndipo aliponijibu huku
kukiwa na ukimya katika gari lile nadhani ni ukweli kwamba kila mmoja alitaka
kujua kuwa nini kiliulizwa, akiwa na tabasamu akanijibu na kusema kaka zile
siyo bangi ila ni zao la biashara huku kwetu kusini la ufuta. Ilikuwa ni kipindi
cha masika nikiwa safarini kwenda Tandahimba kwa mara ya kwanza kwani nilikuwa
mgeni bado Mkoani Mtwara nikitokea Dar es salaam.
Ama kweli kutokujua ni kama usiku wa kiza ufuta
ninaufahamu lakini shina lake nilikuwa sijawahi kuliona ndiyo kwanza hivi leo,
lakini bado haliondoi ukweli wa kufanana na mmea wa bangi haswa ukiutazama kwa
mbali kama ilivyokuwa kwangu nikiwa ndani ya gari.
Hivi karibuni nilifanya ziara ya kutembelea kituo
hicho cha utafiti na safari yangu kituoni hapo nilitaka kwenda kufuatilia zao
la muhogo kama linaweza kuwa zao la kutegemea kwa kuokoa jamii kwa chakula.
Baada ya kuliona shamba lile ambalo bado
halijaandaliwa kwa kilimo kwa sasa, ikabidi nibadili kibao pale pale baada ya
kukumbuka kituko kile cha siku nasafiri kwenda Tandahimba nilipo ufananisha
mmea wa ufuta na bangi nikajiambia itabidi nianze na zao hilo la ufuta kwanza.
Nilianza safari yangu asubuhi kutoka Mtwara mjini kuelekea
kituoni hapo baada ya kukaribia kituo hicho cha utafiti nilishitushwa na sauti
ya konda ikisema risechi wapo? maana yake ni kituo cha utafiti kwa hiyo wao wanafupisha
kwa kuita hivyo tena kwa Kiswanglishi? Nikaitikia kwa nguvu kidogo tupo shusha
kitendo kilichofanya abiria wengine kunigeukia na kunikodolea macho.
Ni sehemu iliyotambalale lakini imesongwa na vichaka
vya miti ya asili kiasi kwamba huweza kuyaona majengo ukiwa mbali hadi ufike
usawa kituo kilipo na katika mlango wa kuingilia kuna bango kubwa la mbao
lililoandikwa Kituo cha utafiti wa kilimo na mifugo Naliendele Mtwara.
Nikaingia getini na kukutana na wazee wawili ambao
nilihisi kabisa ndiyo wanaoshughulika na masuala ya ulinzi mlangoni hapo lakini
pia wanatumika kama wapokeaji wa kuwaelekeza wageni kwenda sehemu ambayo ndiyo
mahususi kwa mapokezi ya wageni na kuwakaribisha kwa kuwaelekeza kama wenyeji
wao kituoni hapo wapo kazini au la.
Kama ilivyoada na mimi pia nikaelekezwa kwenda
mapokezi nilikutana na mtu wa hapo ambapo nikamweleza kama naweza kuonana na
mwenyeji wangu ambaye anahusika na zao la biashara la ufuta.
Ndipo nilipoambiwa yupo na ni Dkt.Omari Mponda
ambaye ni mtafiti wa mbegu bora za mafuta kituoni hapo, ambapo lengo likiwa niweze
kuzungumza naye kuhusiana na mmea ule niliouona kipindi hicho nasafiri na
kuufananisha na mmea hatari wa bangi maana baada ya kudadisi pale mapokezi
nikaambiwa yeye ndiye muhusika wa zao hilo.
Kijana wa mapokeza akaniambia nimfuate basi
nikafanya hivyo ambapo akanipeleka katika jengo moja dogo jipya ambalo
lilionyesha kuwa ndiyo kwanza linaanza kutumika baada ya kumalizika.
Nilipokelewa vizuri na Dkt.Mponda ambaye kichwa
chake kinapendeza kwa kuwa na mvi nyingi zilizoota bila kuacha madoa meusi kiasi
kwamba unaweza kufikiri amemwagiwa unga kichwani ambapo zikionyesha kuwa
ameshaukula chumvi nyingi kidogo, lakini kinachomsaidia ni kuwa mcheshi na
anaonekana mwongeaji na mwenye kujiamini akiwa katika anga zake za kazi na
kumficha hali yake hiyo ya uzee.
Karibu kijana Mimi naitwa Dkt.Mponda mtafiti wa
mbegu bora za mafuta kituoni hapa. Asante mzee Mimi naitwa Bw.Godwin Msalichuma
ni mwandishi wa habari nimekuja tuzungumze kuhusiana na zao la ufuta kwa ujumla
katika kumwendeleza mwananchi wa kusini kiuchumi kwani nimeambiwa hapo nje kuwa
ni zao la biashara kwa upande wa ukanda huu wa kusini.
Dkt.Mponda alianza kwa kutoa historia kidogo ya
kituo cha utafiti Naliendele kwa kusema kuwa shughuli za tafiti za kilimo
zilianza wakati wa ukoloni ambapo waliweka kituo Wilaya ya Nachingwea Mkoani
Lindi na baada ya uhuru zilihamishiwa Ilonga Morogoro na hatimaye Mtwara mwaka
1978, ambapo mwaka 1983 tulikuwa na mbegu bora aina sita ambazo tulikuwa
tumezifanyia utafiti na kushauri wakulima waweze kuzitumia mashambani.
Mwaka 1992 tulitafiti na kupata mbegu bora ya ufuta
tuliyoipa jina la Naliendele 92 ambayo inazaa vizuri zaidi ya mbegu za awali,
tukaendelea na tafiti ambapo mwaka 1994 tulikuwa na mbegu za aina mbili yaani
zawadi 94 na Ziada 94 hizi tuliziingiza kwa ajili ya kuuza nchi za nje zaidi
kuliko matumizi ya hapa nchini.
Tukaendelea na tafiti ambapo mwaka 2002 tukaingiza
mbegu inayoitwa Lindi 2002 ambayo mpaka sasa inatumiwa na wakulima, sifa zake
ni kwamba inavumilia sana magonjwa, ina vikonyo virefu ambavyo vina mifuko ya kubebea
mbegu sita badala ya mbegu zingine kuwa na mifuko ya kubebea mbegu minne tu.
Mbegu hii ilionekana kupendwa sana kwani tulipata
maombi kutoka hata Mikoa ya Rukwa maeneo ya Mpanda na Mbeya katika maeneo ya
Chunya na huku bado inaendelea kufanya vizuri katika kumwendeleza mwananchi
kiuchumi.
Mwaka jana tukaingiza mbegu nyingine iitwayo Mtwara
2009 ambayo sifa zake ni kwamba inatoa mafuta mengi na kiurahisi sana wakati wa
kukamua kwa kutumia LAM PRESS mashine ndogo za kusukuma kwa mkono ambazo
tunashauri wakulima wadogo wadogo vijijini kutumia.
Anasema kuwa ndiyo maana tunawashuri wajasiriamali
wa kati na wadogo kujiingiza katika kuyaongezea thamani kabla ya kuuza nje
yakiwa ghafi haswa kukamua aina hii ya mbegu kwani ina mafuta mengi na ni
rahisi kukamua.
Wajasiriamali wakigeukia zao hili linaweza kuwapatia
kipato kwa haraka kuliko kung’ang’ania zao la korosho ambalo gharama zake za
uzalishaji ni kubwa na bei yake ni ndogo ukilinganisha na ufuta ambao kilo moja
kwa sasa inifika mpaka sh.1, 200 na ukisindika mafuta yanauzwa mpaka sh.5,000
kwa lita moja.
Dkt. Mponda anasema kuwa soko la ufuta ni kubwa sana
na linahitaji kiwango cha tani nyingi kuweza kulitoshereza hivyo kujikuta kuwa
ufuta unaweza ukatoa ajira kwa wananchi wengi zaidi katika kulima na hata katika
kusindika mafuta ili kuliongezea thamani kabla ya kuuza katika soko la nje.
“Ninashauri wajasiriamali kujiingiza katika kulima
na kusindika ufuta kwani wataweza kupata faida kubwa kwa muda mfupi zaidi
kuliko kukimbilia mazao mengine kwa mazoea tu kama korosho lakini mwisho wa
siku hayana tija kama lilivyo hili zao” alisema na kuongeza.
“Unaposindika ufuta hata mabaki yake ni biashara
kwenye upande wa mifugo, kwahiyo unakuta mafuta unauza na mabaki unayauza pia….na
kwa mkulima unaweza kuanzisha ufugaji wako mwenyewe hivyo kuboresha maisha
yako ”. Alisema mtafiti huyo.
Alisema kuwa ufuta una wadudu ambao huwa wanasumbua
na kushaumbulia wakati ukiwa shambani lakini ukifuata ushauri wa kutumia mbegu
bora na kanuni za ukulima wa kisasa na kupata madawa ya kupulizia katika hekta
moja unaweza kuvuna tani 1.5 ambapo
hicho ni kiwango kizuri cha mapato.
Anatoa ushauri kuwa kabla hawajajiingiza katika
kilimo hiki cha ufuta wanaombwa kuja kuwaona watafiti ili kuweza kupata
mahitaji ya kitalaamu ya uzalishaji wa zao hilo na pia kupata historia ya
ukulima bora kutoka kwa wakulima wengine kwani vyote vinapatikana hapo kituoni.
Hakusita kuificha furaha yake ya kutembelewa na
mwandishi wa habari kituoni hapo kwani aliona kuwa na mwanahabari pale ni njia
mojawapo ya matokeo yao ya tafiti yanaweza kuwafikia wananchi waliowengi zaidi
hivyo kumkaribisha tena kuja kupata matokea mbalimbali ya tafiti zinazokuja.
Mwandishi wa makala haya alijaribu kumwuliza kuhusu
jamii inayozunguka kituo hicho inanufaika vipi na tafiti mbalimbali ambazo
zinafanyika kituoni hapo, naye alisema zaidi ya kunufaika na kazi za vibarua
zinazopatikana pale huwa hawajisumbui katika masuala mazima ya ukulima kwani ni
kwa uchache sana katika mazao ya muhogo na korosho ndiyo wanayojishughulisha
nayo.
“Wengi wanaotuzunguka hapa wanaridhika na vibarua
wanavyopata hapa hivyo hawajisumbui kabisa katika ukulima wa mazao haya
tunayoyafanyia tafiti hapa…kwahiyo waandishi mtakapowaelimisha wanaweza
kubadilika na kutambua faida ya kuwa karibu na kituo cha utafiti” alisema
Dkt.Mponda.
Mbali na kufanya tafiti za mbegu bora lakini pia
wanatoa ushauri wa masoko na panapolazimika huwatafutia wakulima wanaozalisha
mbegu bora kupata sehemu za kuuzia mazao yao hayo kwani pia kituo kinatoa
mafunzo kwa wakulima kuzalisha mbegu bora ili kuwauzia wenzao kipindi cha msimu
wa mvua.
Jukumu hili la kuwaelimisha wananchi watafiti
wanashauri lisiachiwe wanahabari na vyombo vyao bali pia hata halmashauri
zinatakiwa kuandaa mipango ya kuwaelimisha wananchi kuchangamkia matokeo ya tafiti
mbalimbali za kilimo.
Kwani halmashauri nyingi hapa nchini zinanufaika na
ushuru wa mazao yanayolimwa katika maeneo yao hivyo wanaombwa kusaidia katika
msukumo ili wanapowakata wakulima basi nao wawe wamechangia katika mapato hayo
yanayoendeleza taifa letu kimiundombinu.