My Blog List

Sunday, July 8, 2012

WAKULIMA WA KOROSHO KUREJESHEWA FEDHA

Na Godwin Msalichuma,
 Masasi
 
SERIKALI imetakiwa kuwarejeshea fedha walizochangia kwa ajili ya ununuzi wa pembejeo msimu uliopita wakulima wa korosho wa wilaya ya Masasi, Mkoani Mtwara baada ya kushindwa kuwasambazia pemebejeo hizo kwa wakati.
 
Uamuzi huo umefikiwa mwishoni mwa hivi karibuni katika kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri hiyo, kilichoketi mjini Masasi, baada ya kupokea taarifa ya hali ya upatikanaji wa pembejeo iliyowasilishwa na ofisa kilimo na mifugo wa Wilaya hiyo, Bw.Mashaka Mfaume.
 
Katika taarifa yake Bw. Mfaume alikieleza kikao hicho kuwa wakulima wa Wilaya hiyo wanahitaji sulfa ya unga 592.39 tani na dawa za maji lita 48,813 mahitaji ambayo yalikadiriwa na mfuko wa kusimamia pembejeo nchini (WAKIF).
 
“Hadi sasa  ni sulfa ya unga tani 84.3 sawa na asilimia 14 ya mahitaji na lita 13,103 za dawa za maji sawa na asilimia 78.19 tu ya pembejeo za korosho ndizo zilizowafikia wakulima, licha ya msimu wa mahitaji ya dawa hizo kuwadia” alisema ofisa huyo.
 
Aliongeza kuwa “Wakulima wa wilaya ya Masasi katika msimu uliopita kupitia makato ya sh. 30 kwa kilo ya korosho waliyouza walichangia zaidi ya sh. 633,922,830 kwa ajili ya pembejeo…mikorosho imechipua na uhakika wa kuzipata pembejeo kwa wakati haupo” alisema Bw. Mfaume.
 
Alisema kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wakifu kwa halmashauri hiyo, pembejeo za zao hilo zinatarajia kuingia nchini wiki mbili tangu Juni, 22 mwaka huu.
 
Taarifa hiyo iliibua hisia za madiwani hao na kuitaka serikali kurejesha fedha zilizochangiwa na wakulima haraka sana ili waweze kununua pembejeo maeneo mengine.
 
“Serikali imeshindwa kutimiza wajibu wake, sasa tunaomba fedha ambazo wakulima wamechangia warejeshewe…na kuanzia sasa makato ya lazima ya fedha hizi yasimame …wakulima sasa watachangia kwa hiyari yao ” alisema Bw. Albert Mlambala diwani wa kata ya Mtandi.
 
Naye diwani wa kata ya Nanjota Bw. Edward Mmavele aliitaka serikali kuanza malipo hayo mapema Julai, 2 mwaka huu huku akilaani utendaji kazi wa serikali uliowafikisha katika hali hiyo.
 
“Kwanini mnatunyanyasa wakulima..tunaomba pesa hii irudi..kwa hili habari ya serikali naomba tusisikilize, na sisi ni mamlaka…naomba mwenyekiti udhihirishe uwenyekiti wako kwa kuhakikisha fedha hizi zinarudi haraka inavyowezekana” alisema Bw. Mmavele huku akishangiliwa na madiwani wenzake.
 
Diwani wa kata ya Mnavira, Bi. Johari Chilumba alienda mbali kwa kuitaka serikali kuwalipa fidia wakulima wa korosho kutokana na hasara wanayopata kwa serikali kuchelewesha pembejeo za zao hilo na kudai kuwa hata zile walizoletewa hazifai kwa matumizi.
 
Akihitimisha hoja hiyo mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Bw. Jafari Mkwanda alikubaliana na hoja za wajumbe hao za kuitaka serikali kurejesha fedha za wakulima na kwamba nguvu sasa itawekezwa katika kuimarisha mfuko wa pembejeo wa Wilaya hiyo.
 
“Wote waliosababisha tatizo hili wawaombe radhi wakulima wa korosho, tena kwa maandishi ili ifahamike wazi kuwa si halmashauri iliyosababisha hali hii” alisema Bw. Mkwanda