Mwenyekiti wa chama cha mapinduzi katika halmashauri ya manispaa ya Mtwara akiongea kusisitiza jambo katika baraza la madiwani.
MSIANDIKE HABARI ZA MABAYA TU
Na Godwin Msalichuma,
Mtwara,
WAANDISHI wa habari katika Manispaa ya Mtwara
Mikindani wameshauriwa kutokuandika habari zinazolenga mabaya tu, waangalie na
mazuri pia yanayofanywa na halmashauri katika kutekeleza ilani ya chama tawala
ili kuweka urari ulio wa haki.
Rai hiyo ilitolewa na mwenyekiti wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM) katika Manispaa hiyo Bw. Yusufu Mineng’ene katika kikao maalum
cha bajeti cha baraza la halmashauri hiyo hivi karibu lililofanyika katika
ukumbi wa Manispaa.
Alisema kuwa anasikitishwa kusikia mara nyingi
habari zinazoandikwa na wanahabari wa Mkoa wa Mtwara ni zile zenye kasoro tu
hata kama kuna ambazo halmashauri na madiwani wake wamefanya vizuri, kwani kama
kuna habari nzuri halmashauri haipaswi kupongezwa aling’aka.
“ Huwa mara nyingi namwambia mke wangu afunge redio
kwani sioni maana ya kusikiliza habari mbaya tu za kuikosoa halmashauri kama
vile hakuna mazuri ambayo yamefanywa….nachukua nafasi hii kuwaomba waandishi wa
habari kuandika mazuri pia yanayofanywa na halmashauri” alisema Bw. Mineng’ene.
Aidha kabla ya kufungwa kwa kikao hicho cha madiwani
naibu meya wa halmashauri ya Manispaa hiyo Bw. Zarari Zarari alirudia Kauli
hiyo ya mwenyekiti wa chama tawala kwa kusema kuwa waandishi kama hawayaoni
mazuri basi wachukue muda wa kutembelea Ofisi ya Meya basi watajulishwa na
kufahamishwa yaliyopo ili wakahabarishe umma.
“Kabla ya kuahirisha kikao hiki naomba kusistiza
zaidi juu ya hili la wanahabari wa Mkoani kwetu kwamba kama hatuyaoni mazuri
basi tembeleeni Ofisi ya Meya kupata ufamisho zaidi wa yale mazuri
tunayoyafanya ili Tujenge Mtwara yetu” alisema Bw. Zarari.