Askari polisi akiwa makini kusimamia ubebaji masanduku ya kura na kwenda kuhesabu |
WAKONGWE WABWAGWA UCHAGUZI
CCM MTWARA
Na Godwin Msalichuma,
Mtwara,
UCHAGUZI wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM) umefanika mwishoni mwa wiki katika
wilaya zote Sita za Mkoa wa Mtwara huku safu ya wenyeviti ikitawaliwa na sura
mpya.
Ni mwenyekiti wa Wilaya ya Masasi
pekee, Bw. Kazumali Malilo aliyeweza kutetea kiti chake kwa kishindo kwa
kumbwaga mpinzani wake Bw. Andrew Kasawala aliyeambulia kura 224, huku yeye
akijizolea kura 1380 kati ya 1604 zilizopingwa.
Nafasi ya ujumbe wa halmashauri kuu
(NEC) katika wilaya hiyo imetwaliwa na Bw. Pole Ramadhani kwa kura 978 baada ya
kumbwaga mpinzani wake Bi. Ketty Kamba aliyepata kura 489.
Katibu wa CCM wa Mkoa wa Mtwara
Alhaji Masoud Mbengule ameiambia Msalichuma Mtwara News
ofisini kwake siku ya Jumapili kuwa uchaguzi huo umepita salama
huku nafasi nyingi za uongozi zikichukuliwa na sura mpya.
Alisema katika wilaya ya Newala, Bw.
Ali Athumani Sadi ametangazwa kuwa mwenyekiti mpya wa chama hicho baada ya
kupata kura 803 dhidi ya mtetezi wa kiti hicho aliyeangukia pua kwa kupata kura
721, huku nafasi ya NEC ikihodhiwa na Bw. George Huruma Mkuchika aliyepata kura
1001 na kuwabwaga Bw. Abdallah Napinda (267) na Shaibu Namkuna (261).
“Tandahimba nafasi ya uwenyekiti
ulirudiwa mara mbili baada ya aliyeongoza kutofikia nusu ya wapiga kura,
ziliporudiwa Bi. Sophia Makonyola aliyekuwa anatetea kiti hicho alipata kura
619 na Bw. Abdul Haji Namtula alipata kura 980, hivyo Bw. Namtula ndiye
mwenyekiti mpya wa CCM Tandahimba” alisema Alhaji Mbengule.
Aliongeza kuwa “Nafsi ya NEC
jumla ya kura 1623, kura 38 ziliharibika…Balozi Rashid Makame kura 995,
Bw. Namyundu Ali Salum kura 419 na Bw. Lihundu Abdallah Samli alipata
kura 171, hivyo M-Nec wa Tandahimba ni Bw. Balozi Makame”.
Alisema Mtwara mjini nafasi ya
uwenyekiti imechukuliwa na Bw. Ali Mussa Chikanwene kwa kura 449 na kumbwaga
mtetezi wa kiti hicho Bw. Yusuf Mineng’ene alipata kura 174, huku Bi. Hawa
Mangasala akiambulia kura 35 na Bw. Bakari Mbwana kura 6kati ya kura 672
zilizopigwa huku 8 zikiharibika.
Katika nafsi ya Nec, Alhaji Mbengule
alisema Bw. Godbless Kweka ameshinda nafasi hiyo kwa kura 373, na kuwabwaga Bw.
Saidi Mussa Swalehe aliyepata kura 247, Bw. Phiri Makaburi (29) na Bw. Ernest
Haule (16) kati ya kura 668 zilizopigwa huku 3 zikiharibika.
Kwa upande wa Mtwara vijijini, Bw.
Ali Komba alimbwaga mtetezi wa kiti cha uwenyekiti Bw. Ahmadi Likomba
baada ya kupata kura 867 kwa 570 kati ya kura 1454 zilizopigwa huku kura 77
zikiharibika.
Aidha kwa upande wa Nec katibu huyo
wa Mkoa alisema Bw. Salehe Livanga aliwabwaga Alhaji Mpeme (390) na Bw.
Salehe Nandieti (156) baada ya kupata kura 816 kati ya 1416 zilizopigwa huku
kura 54 zikiharibika.
“Wilaya ya Nanyumbu kura nafasi ya
uwenyekiti ilirudiwa mara mbili, baada ya marudio matokeo yalikuwa, Bw. Muhata
Masusa kura 407 na Bw. Ali Mohamedi Dua kura 395…mwenyekiti mtetezi Bw.
Chibwana Mtimbe yeye alishindwa mapema” alisema alhaji Mbengule
Aliongeza kuwa “Nec, Bw. Hassan
kambutu alipata kura 426 na kuwashindwa Bw. Rajabu Mrope aliyepata kura 361,
Bw. Linga Idd Mpwanya kura 106 na Bw. Mwema Hassan Issa kura 67…M-Nec hapa ni
Bw. Kambutu…uchaguzi umepita salama na sura mpya kama nilivyokueleza” alimaliza
Bw. Mbengule.
Mwisho
Mwezesheji katika warsha ya siku tatu ya waandishi wa Mtwara juu ya maadili na azimio la Dar es salaam kuhusu uhuru na uwajibikaji wa vyombo vya habari (DEFIR) Deodatus Mfugale akiwa ukumbini |
Waandishi wa habari wa Mkoa wa Mtwara wakiwa katika warsha hiyo |
WASHAURIWA KUZINGATIA MAADILI
Na Godwin Msalichuma,
Mtwara,
WAANDISHI wa habari Mkoani hapa wamekumbushwa
kuzingatia maadili ya kazi yao ili kuweza kuaminika katika kazi zao na jamii
ambayo ndiyo mwajiri wao wa kwanza kiuwajibikaji.
Hayo yamebainishwa juzi katika warsha ya maadili ya
uandishi wa habari pamoja na azimio la Dar es salaam juu ya uhuru na
uwajibikaji wa vyombo vya habari ambayo yanaendelea kwa siku tatu katika ukumbi
wa klabu ya waandishi wa habari ya Mtwara, ambayo yameandaliwa na baraza la
habari la Taifa (MCT).
Bw. Deodatus Mfugale ni mmoja wa wawezeshaji ambaye
alisema kuna umuhimu mkubwa wa kuzingatia maadili ambapo huleta uandishi wa
uwajibikaji, kukuza na kujenga taaluma, na ni mwongozo wa utendaji wa kila siku
wa shughuli za kiuandishi.
Alisema kuwa ukizingatia misingi ya maadili utafanya
kazi za kiuandishi kwa kujitawala mwenyewe bila kusukumwa na mtu mwingine
lakini pia huleta ulinzi katika ufanisi wa maslahi yako na jamii kwa ujumla.
“Ukifanya kazi zako kwa kuzingatia maadili na
misingi yake kunasaidia sana kwanza kukujenga wewe mwenyewe lakini pia jamii
nzima inakuamini na isitoshe chombo unachokifanyia pia kinajenga uaminifu kwako
na kwa jamii kinakuwa kioo chao” alisema Bw. Mfugale.
Aidha awali wakati wa kufungua warsha hiyo mwandishi
nguli wa siku nyingi Bw.Chrysostom Rweyemamu aliwakumbusha waandishi wa habari
wa Mtwara nguzo muhimu katika uandishi wa kuzingatia maadili ambazo alizitaja
baadhi yake ikiwa ni ukweli, urari wa habari, usahihi na kutenda haki siku zote
za kazi zako.
Aliwakumbusha pia kuwa kuna hatari ya uhuru wa
habari kuweza kutoweka iwapo baadhi ya mambo
hayatafuatwa kwa uangalifu mkubwa ambapo miongoni mwayo maslahi duni kwa
waandishi wa habari, kuwa na msimamo usioshaurika kwa viongozi na wamiliki wa
vyombo vya habari, Rushwa, uelewa na ujuzi Mdogo, kufanya urafiki na Vyanzo vya
habari lakini pia kuvunja maadili yenyewe.
Hata hivyo alibainisha kuwa kuna mtanziko na
changamoto wakati wa kupata habari ambapo wakati mwingine mwanahabari unatakiwa
kuwa makini wakati wa kutimiza majukumu yako na kubadilika kutokana na
mazingira unayoyakuta katika eneo la tukio ili uweze kupata habari yako bila
mgongano.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment
Any