ONGEZENI ADHABU KUPUNGUZA UJANGILI
Na Godwin Msalichuma,
Saanane Mwanza,
ADHABU ndogo zinazotolewa kwa majangili wanaojihusisha
na uvuvi haramu wa samaki ni moja
ya changamoto inayoikabili hifadhi tarajiwa ya Saanane iliyoko katika Wilaya ya
Nyamagana Mkoani Mwanza.
Akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea
katika hifadhi tarajiwa hiyo ambayo ina visiwa vitatu kaimu mhifadhi Donatus Bayona alisema kuwa adhabu hizo
hazileti fundisho kwani majangili hayo yanayofanya uhalifu mkubwa unaosababisha
madhara kwa samaki walio ndani ya ziwa Victoria tofauti na adhabu wanazopatiwa.
Bayona alisema kuwa adhabu ndogo zinazotolewa na
mahakama kwa majangili ambao wanapatikana na hatia kwa kufanya uhalifu ndani ya hifadhi hiyo
tarajiwa hazitoi somo kwa jamii na pia haziwezi kumfanya mtu kuacha kuendelea
kufanya uhalifu huo.
“Adhabu za majangili kuwa ndogo bado ni changamoto
kwetu wengi wao kesi zao zinaishia kwa kutozwa faini isiyozidi shilingi 10,000
na hata wanaofungwa ni kifungo cha miezi minne au kifungo cha nje, adhabu hizi
hazimfanyi mtu aache kazi yake pia hazitoi somo katika jamii inayowazunguka”
alisema
Kwa mwaka 2011 alisema jumla ya majangili 12
walikamatwa wakivua samaki kinyume cha sheria ambapo baadhi yao hutumia uvuvi
wa sumu ambao unaleta madhara makubwa kwa samaki walio ziwani.
“Hawa wanaovua samaki kwa njia ya sumu wanaleta
madhara makubwa kwakua wanaua mazalia ya samaki hali inayochangia kutokuwa na
uhifadhi endelevu kama yalivyo malengo ya hifadhi tarajiwa” alisema.
Kaimu mhifadhi huyo alisema kwasasa wanatoa elimu ya
uhifadhi kwa jamii kwa ushirikiano na jeshi la polisi na Idara ya uvuvi Mkoani
Mwanza ili kuwezesha jamii kushiriki katika swala zima la uhifadhi wa
rasilimali hizo.
Hifadhi tarajiwa hiyo yenye Ukubwa wa km 2.1 ilianza
mwaka 1964 ikiwa bustani ya wanyama
chini ya Wizara ya Maliasili na baadae mwaka 1991 ikawa pori la akiba na sasa iko chini ya TANAPA ikiwa katika
Mchakato wa kuwa hifadhi Kamili.
Mwisho.