WALIMU 3,000 WAHITIMU
CHUO KIKUU HURIA TANZANIA
WALIMU 3,000 wamehitimu ualimu kupitia mpango wa elimu kwa
masafa marefu katika miaka mitano iliyopita, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Profesa Tolly
Mbwete amesema.
Alitangaza hayo jana Jijini Dar es Salaam wakati wa kutia
saini mkataba wa ushirikiano (MoU) kati ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT)
na Sektretarieti ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) unaoikifanya
chuo hicho kuwa Kituo cha Mafunzo ya elimu kwa masafa kwa walimu SADC. Alitia
saini na Mratibu wa Mradi huo wa SADC –ODL, Thulanganyo Thutosile
aliyemwakilisha Katibu Mkuu wa SADC.
“OUT iko katika nafasi nzuri ya kutekeleza mipango ya
maendeleo ya ODL (elimu kwa masafa marefu) katika sekta zote ambazo zinaikubali
elimu na mafunzo kama nyenzo muhimu
katika maendeleo ya taasisi na jamii.
…Walimu ni wahandisi wa maendeleo ya fikra sehemu yoyote
ile. OUT ina uzoefu katika utoaji mafunzo kwa masafa (ODL) na elimu kwa walimu
ikiwa imetoa walimu 3,000 waliosoma kwa masafa (ODL) katika miaka mitano
iliyopita., “ Profesa Mbwete alisema katika hafla hiyo chuoni OUT Kinondoni
Biafra.
Alisema, mbali ya SADC kuifanya OUT kituo cha mafunzo kwa
masafa kwa walimu wanaojiendeleza kwa nchi zote 9 wanachama wa SADC, pia
Sekreatrieti hiyo imeipa OUT, majukumu ya
kusimamia mfumo wa menejimenti ya
maarifa ambapo mfumo wa kompyuta wa kuftekeleza hilo utafungwa chuoni hapo.
Profesa Mbwete alisema OUT kama kituo teule cha SADC kwa
mafunzo ya masafa kwa walimu kuanzia wa shule za msingi hadi vyuo vikuu
kitakuwa kikitoa kozi za muda mfupi na za muda mrefu kwa walimu na watunga
sera, na watoa mafunzo kwa walimu wanaosoma kupitia ODL ili kuwapa maarifa na
ujuzi
Alisema OUT ambayo mwaka huu inatimiza miaka 20 tangu
ianzishwe, imepewa uwezo wa
kuendesha kuanzia mwezi ujao, mafunzo
kwa wataalam wa kutoa mafunzo ya masafa marefu (ODL) kwa ngazi za stashahada na
shahada za uzamili kutoka kwa walimu wanaotaka kusoma kutoka katika nchi za
SADC . Mafunzo hayo yatatolewa katika Taasisi ya Elimu Endelevu (ICE) na Kitivo
cha Elimu OUT, Kinondoni.
Utiaji saini huo ulishuhudiwa na mwakilishi wa Wizara ya
Elimu na Mafunzi ya Ufundi Stadi, A Kajigili ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu
anayeshughulikia elimu ya juu. Kajigili katika hotuba yake alisifu mpango huo
akisema utakuwa wa manufaa makubwa kwa maendeleo ya elimu kwa nchi za SADC.
Alisema kwa kuwekeza katika elimu kwa walimu, kituo hicho
cha elimu kwa walimu kupitia masafa, SADC imeonesha inavyothamini umuhimu wa
walimu katika jitihda za kuinua kiwango cha elimu SADC.
“Kuna program nyingi za elimu kwa walimu kwa masafa
zinazotolewa katika nchi wanachama wa SADC lakini ni walimu wachache wenye
uwezo na ujuzi unaotakiwa. Ni muhimu kuhakikisha kuwa wanaotoa elimu kwa masafa
(ODL ) wanahakikisha wanakitutimia kituo hiki kujipatia maarifa sahihi, ujuzi
na stadi vitakavyowasaidia kuwa na ufanisi, weledi katika utoaji wa mafunzo
hayo kwa njia ya ODl, “ alisema Kajigili.
Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa SADC, Thulanganyo alisema
utiaji saini huo unahitimisha wazo la kuanzishwa kwa kituo hicho la tangu mwaka
2009 na kwamba huu ni mwanzo wa mafanikio makubwa zaidi katika elimu kupitia
kwa wadau ikiwemo Benki ya Maendeleo Afrika (ADB) inayougharimia. Alisema
anatumaini nchi wanachama zitawaruhusu walimu wao kujiendeleza kupitia ODL na
SADC itasaidia zaidi.
Habari hizi kwa msaada wa Godfrey Lutego