My Blog List

Saturday, June 19, 2010

Kutoka Mtwara

SISI KWA SISI NA TUMAINI WAJIIMARISHA NA UNENEPESHAJI KAA

Na Godwin Msalichuma,
Mtwara.

WAKAZI wa Mtaa wa Miseti kata ya Chuno na Mangowera katika halmashauri ya Manispaa ya Mtwara, wanaounda vikundi vya SISI KWA SISI na kile cha TUMAINI ni ambavyo vimepata fedha za kuendesha miradi ya jamii kupitia mfuko wa maendeleo ya jamii (TASAF), katika kutekeleza miradi ya unenepeshaji wa Kaa.

Vikundi hivyo vinavyoundwa na wanchama 23 kwa SISI KWA SISI na 22 kwa TUMAINI, awali walikuwa wanafanya shughuli za uvuvi wa mtu mmoja mmoja na usiozingatia utunzaji wa mazingira na rasilimali za taifa, na kwa wanawake walikuwa wanajihusisha na uchuuzi wa samaki baada ya wanaume kurudi kutoka baharini.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na mwandishi wa habari hizi aliyewatembelea maeneo ambako miradi hiyo inatekelezwa walisema wanaipongeza serikali kupitia (TASAF) kwani fedha walizozipata kwa ajili ya kuendeshea miradi yao imewafaa na kuweza kuwaongezea vipato katika kaya zao hivi sasa.

“Ndugu mwandishi fedha hizi zinatusogeza na hawa kaa tunaowapanda hapa mara nyingine tunaenda na hawa wanaume usiku kuvua kwa ajili ya mbegu na tukikosa huwa tunanunua mmoja shilingi 500” alisema Bi.Mwanashuru Mzee mwenyekiti wa kikundi cha SISI KWA SISI mtaa wa Miseti kata ya Chuno.

Bi.Mzee alisema kuwa (TASAF) imeweza kuwapatia kiasi cha shilingi milioni 9,835,000 ambazo wameweza kutengeneza vijaruba 43 katika shamba lao la kunenepesha kaa amabapo kila kijaruba kina vizimba 10 na kila kizimba kinauwezo wa kufuga kaa mmoja, mpaka sasa wanavizimba 9 vyenye jumla ya kaa 90, lengo lao ni kufikisha kaa 100.

“Tunawanenepesha hawa kaa kwa muda wa miezi mitatu ambapo wakifikisha uzito wa kilo moja na nusu wanakuwa tayari kwa kuuzwa kwa wateja wetu kwa bei ya shilingi 5,000 mpaka shilingi 6,000…hatuna uhakika na soko lakini (TASAF) wameahidi kutusaidia katika hilo na kuna mteja mmoja ametuahidi kunua pindi watakapofikisha uzito huo” alisema Bi.Mzee.

Aliishukuru serikali kwa niaba ya kikundi kupitia (TASAF) kwani wanaonyesha ushirikiano na vikundi vya jamii katika uzalishaji mali kama vya kwao na vingine hapa nchini,lakini aliomba elimu kutolewa zaidi juu ya ufugaji na unenepeshaji wa kaa pamoja na utunzaji wake.

Kikundi hicho kilianzishwa mwaka jana na kufanikiwa pia kuanza kazi ya unenepeshaji kaa na utunzaji, kina jumla ya wanachama 23 kati yao wanaume ni 19 na wanawake 4, awali walikuwa na kipato kidogo na cha mtu mmoja mmoja lakini katika kujiunga katika vikundi kunaleta tija hata kipato kukua zaidi aliongeza mwenyekiti huyo.

Kwa upande wa kikundi cha TUMAINI Bw.Juma Mbaruku kilichopo Mangowera wao wanasema mwelekeo wa maisha yao kwa sasa unakuwa mzuri na kipato wanauhakika kitapanda ukilinganisha na hapo awali.

Kwa mujibu wa mwenyekiti wa kikundi hiki wao walipata fedha kutoka TASAF kiasi cha shilingi milioni 9,262,100 ambapo wana idadi ya vijaruba 43 vyenye jumla ya vizimba 430 na mpaka sasa vizimba vyenye kaa ni 27 ambapo jumla ya kaa wanaonenepeshwa na kikundi chake ni 270.

“Mpaka sasa tuna kaa 270 tunaowanenepesha, lakini tunasikitika kusema kwakuwa kazi hii ni mara yetu ya kwanza kuifanya, tunakumbwa na tatizo la kutoroka kwa kaa kupitia matundu ya vijaruba kama mnavyoona ……lakini tunajitahidi kupambana na hali hiyo naamini tutashinda na kufikia malengo yetu tuliyojipangia”alisema Bw.Mbaruku.

Bw.Mbaruku alisema kikundi chao kilianzishwa mwaka jana na kina jumla ya wanakikundi 22 kati yao wanaume ni 11 na wanawake 11 amabao wanatoka katika jamii inayoishi katika mazingira magumu ya pwani ya bahari ya Hindi.

Alitoa mwito kwa serikali kupitia (TASAF) kama kunauwezekano wa kuongeza katika bajeti za miradi ziada kidogo kwani kama tatizo linalowakabiri la kutorokewa na kaa kurudi baharini, wanakosa fedha za kununulia wengine na kuwa idadi ya kaa inapungua bila wao kuwaongeza kwakuwa wao wanategemea kununua.

“Wito wangu kwa serikali kama wanaweza kutuongezea fedha kupitia bajeti zao….au kama wanaweza kutushirikisha katika kupanga bajeti husika, kwani kuna matatizo mengine yanakuwa hayawekewi na baadaye yanajitokeza…kama hili la kaa kutoroka” alisema Bw.Mbaruku.

Mwisho.

TASAF YASAIDIA KUIMARISHA UVUVI MANISPAA MTWARA

Na Godwin Msalichuma,
Mtwara.

ZANA bora na madhubuti za uvuvi ambazo wananchi wa halmashauri ya manispaa ya Mtwara kutoka katika vikunndi vya UVUVI WA SAMAKI MADABA, KAZI YA MUNGU,CHUNO UVUVI GROUP na MWELEKEO GROUP SHANGANI WEST wamezipata kupitia mfuko wa maendeleo ya jamii (TASAF) ili kutekeleza na kuimarisha uvuvi endelevu na kukuza vipato vya kaya na familia zao.

Miradi hiyo ya uvuvi katika halmashauri ya manispaa ya Mtwara iliyopata ufadhili kutoka katika mfuko wa maendeleo ya jamii TASAF ili waweze kujikwamua na kufanya uvuvi usiokuwa na madhara kwa mazingira na viumbe baharini na pia kujitoa katika hali duni wanayopitia kimaisha.

Wakiongea kwa nyakati tofauti katika miradi yao baada ya kutembelewa na mwandishi wa habari hizi, waliipongeza serikali kupitia mfuko wa maendeleo ya jamii (TASAF) kwa jitihada zake za kuwainua katika miradi wanaiibua kutoka katika maeneo yao wanayoishi.

“ Ninashukuru kuwa serikali yetu inatukumbuka na kutupatia miradi kama hii ya uvuvi wa kutumia vyombo na zana zinazokubalika…kwani awali tulikuwa tunapata shida kabla ya kupata mradi huu…kila mmoja alikuwa anavua kwa kutumia mtumbwi na nyavu ambazo zilikuwa hazina viwango wala utunzaji wa mazingira na viumbe wenyewe”alisema Bw.Said Ahmadi mwenyekiti wa kikundi cha uvuvi wa samaki Madaba.

Bw.Ahmadi alisema kuwa kikundi chake kilianza mwaka jana na kina idadi ya wanachama 17 mchanganyiko wa wanaume 9 na wanawake 8, na mfuko wa maendeleo ya jamii (TASAF) uliwapatia kiasi cha shilingi milioni 16 ambazo wamezitumia kupata zana za uhakika wakiepuka kufanya uvuvi wa awali wa mmoja mmoja na wakutumia mitumbwi na vifaa duni.

Kwa upande wa kikundi cha uvuvi Kazi ya Mungu kilichopo kata ya Chuno mfuko wa maendeleo ya jamii (TASAF) umewawezesha kiasi cha shilingi milioni 17 ambapo kikundi kilianzishwa mwaka jana pia kikiwa na idadi ya wanachama 10 kati ya hao 5 ni wanawake na 5 ni wanaume.

Wakiwa na furaha kubwa kwa kutembelewa na mwandishi wa habari hizi, wakiwa wenye kujiamini kabisa walisema kuwa mradi una matumaini makubwa ya kuwanuifaisha kimapato na kimaisha kuliko ilivyokuwa mwanzo kabla ya mradi huu wa maendeleo ya jamii (TASAF) kwawezesha kifedha.

Mwenyekiti wa kikundi cha Chuno uvuvi group Bw.Said Abdalla hakusita kuionyesha furaha yake mbele ya mwandishi wa habari hizi kwa kusema kuwa kutembelewa na kuona miradi yao ya maendeleo ya kijamii ni faraja kwao.

“Nadhani ni faraja kubwa mwandishi kwanza ndio kwanza ninarudi kutoka Pemba Mikindani kuangalia maendeleo ya mashua yetu ya uvuvi tunayoimalizia kutengeneza baada ya kupatiwa fedha na (TASAF), ambapo tulipewa kiasi cha shilingi milioni 18 ambazo baadhi tumezitumia kwa mafunzo na zingine ni kwa ajili ya vifaa vya uvuvi endelevu.

Bw.Abdalla alisema kikundi chake kilianza mwaka jana na kina idadi ya wanachama 23 mchanganyiko lakini hakuweza kubainisha kuwa uwiano ukoje kati ya wanaume na wanawake na anafurahishwa na serikali kuwajali wananchi wake kupitia mfuko wa maendeleo ya jamii (TASAF) ambao anauhakika kuwa kipato cha kaya kitapanda ukilinganisha na awali kabla ya kupata mradi huo.

Mwelekeo group ni miongoni mwa vikundi vilivyotembelewa na mwandishi wa habari hizi na kimenuifaka na fedha kupitia mfuko wa maendeleo ya jamii TASAF ambacho kipo Shangani West katika manispaa ya Mtwara na walimweleza mwandishi kuwa wamewezeshwa kiasi cha shilingi milioni 16.6 ambazo wamenunua boti na vifaa vingine vya uvuvi.

“Kikundi chetu kilianza mwaka juzi na kina idadi ya wanachama 16, wanawake 6 na wanaume 10 ambao tulitoka katika uvuvi mdogo mdogo wa kutumia mitumbwi na zana zisizofaa kwa mazingira na viumbe baharini…tunaishukuru serikali kwani tumepata chombo hiki na tumeshaanza majaribio ya kukitumia pamoja na zana zingine za uvuvi”alisema Bw.Bakari Said mwenyekiti wa kikundi hicho.

Mwisho.


SERIKALI YASHAURIWA KUELIMISHA KWANZA

Na Godwin Msalichuma,
Mtwara,

SERIKALI imeshauriwa kuwa iwe ianatoa mafunzo zaidi kwa wananchi kujitambua kabla ya kuwakabidhi fedha kwa ajili ya uendeshaji wa miradi ya maendleo ya jamii ili kuwajengea uwezo wajitambue na kuweza kujua namna ya kuzitumia zeweze kuwasaidia.

Ushauri huo ulitolewa nyakati tofauti na baadhi ya wanufaika wa fedha za maendeleo ya jamii (TASAF) walipotembelewa katika miradi yao na mwandishi wa habari hizi, aliyesisi zaidi alikuwa ni Bw.Saidi Malebo wa kikundi cha TUWENAO VVU GROUP ni waathirika wa vvu wanaoishi kwa matumaini maeneo ya Mdenga katika manispaa ya Mtwara.

Bw. Malebo alisema kikundi chake kilianzishwa miaka mitatu iliyopita wakiwa na lengo la kufuga kuku, lakini malengo yao hayakuweza kutimia kutokana na sababu mbalimbali ambazo hakuweza kuzitaja na kina idadi ya wanachama 32 ambao wote ni waathirika wa vvu.

“Unajua watu kama sisi serikali inabidi kutoa elimu ya kutosha juu ya kujitambua…kwani ikitoa tu fedha bila mkazo zaidi unavyojua tuna matatizo mengi kwahiyo unaweza kukuta mwisho wa siku watu wakaona kuwa fedha walizozipata zinafaa kugawana kwa ajili ya kutatua matatizo yao binafsi”alisema Bw. Malebo.

Alisema kwa sasa wamebakia wanachama 18 ambao wapo wanaendelea na ufugaji wa mbuzi wa asili baada ya kupata fedha kupitia mfuko wa maendelao ya jamii (TASAF), na ni baada ya kushindwa kutekeleza mradi wa kwanza wa kufuga kuku.

Aliongeza kwa kusema kuwa jamii ikielimishwa kujitambua zaidi inaweza kupiga hatua kimaendeleo, zaidi ya kupewa fedha alisema usipojitambua itakuwa kazi bure kwani unaweza kushindwa kufanya chochote na baadaye zinaweza kuyeyuka tu bila mafanikio.

Alisema kuwa kikundi chake kimepata fedha kupitia mfuko wa maendeleo ya jamii (TASAF) kiasi cha shilingi milioni 11.4 ambazo wazitumia kununua mbuzi 50 kati ya hao 4 ni madume na kiasi hicho hicho watakitumia kununua vyakula vya mbuzi hao zaidi ya malisho ya kawaida ya majani.

Bw.Malebo alimalizia kwa kusema naishukuru serikali kwa kutoa fedha za miradi hii ya jamii kwani inawasaidia katika kujikwamua katika hali za kimaisha na kukuza vipato vya kaya zao na familia, na kuongeza kuwa serikali iongeze bidii kuwajali watu katika vikunda mbalimbali hapa nchini.

Mwisho.

KIKUNDI SHIRIKISHI WANEEMEKA NA MRADI WA NYUKI

Na Godwin Msalichuma,
Mtwara,

MRADI wa ufugaji wa nyuki katika kikundi SHIRIKISHI kilichopo Mikindani katika halmashauri ya Mtwara katika kata ya Kisungule ambacho kinawanufaisha wanachama idadi yao ikiwa 19, kati yao wanawake ni 13 na wanaume 6, waliojidhatiti kwelikweli kuufukuza umasikini.

Kwa mujibu wa mwenyekiti wa kikundi Bi.Fatuma Bakari alisema wakati akiongea na mwandishi wa habari hizi katika maeneo ya shamba lao la nyuki lilipo Mikindani, kuwa kilianza mwaka jana baada ya kukusanyika wakitokea kila mmoja kufanya shughuli zake mmoja mmoja ambapo tija ilikuwa haieleweki wala hakukua na mshikamano.

“Kwa kweli hapo awali tulikuwa tumetawanyika na kila mmoja alikuwa na shughuli zake binafsi ambazo hazikuwa na faida maana nguvu ya mtu mmoja si kama ya sasa tulivyowengi…ukiwa peke yako huwezi kulala eneo kama hili hapa kwa ajili ya kuwahamisha nyuki na kuwapeleka katika shamba letu jingine”alisema Bi.Bakari hapo shambani msituni.

Alisema kuwa mfuko wa maendeleo ya jamii (TASAF) umewawezesha kwa kuwapatia kiasi cha shilingi milioni 12, ambazo wameweza kununua mizinga 50 na lengo lao kuwa nayo 100, pia wameweza kupata vifaa mbalimbali vinavyohitajika katika masuala ya ufugaji wa nyuki.

Kwa upande wa masoko ya asali wameahidiwa na wataalamu kuwa wakishafikia kipindi cha mavuno wataletewa wateja wa uhakika wa kuweza kununua asali yao kwa kiasi kikubwa, alisema pia kuna mahitaji makubwa tu ya asali katika soko la ndani ambalo kwa lita moja unaweza kuuza kwa shilingi 3,000 mpaka 3,500.

“Tumeelezwa na mtalaam wa nyuki kuwa baada ya miezi sita tunaweza kuvuna kwa awamu ya kwanza…..lakini baada ya awamu hiyo ni baada ya miezi minne unavuna asali na tunategemea kila mzinga kutoa kiasi cha lita 50 na zaidi kama utalaam utatumika”alisema na kujigamba Bi.Bakari.

Bi.Bakari alisema kuwa baadhi ya vifaa vingine walivyokwisha kuvinunua ni pamoja na ndoo, madramu ya plastiki, nguo za kuvunia pamoja na kofia za kufunika uso, vitu vingine ni mabomba ya moshi na mapipa ya kuchemshia n’ta.

Mwishoni aliishukuru serikali kupitia mfuko wa maendeleo ya jamii (TASAF) kwa jitihada zao za kuhakikisha kuwa fedha wanazopewa zinafika kwa walengwa ambao ni wao na wengine sehemu mbalimbali inakoendeshwa miradi ya jamii kama ya kwao, ila ameuomba mfuko kutokuchelewesha fedha kipindi wakiona mradi unafaa na wakisha ukagua.

Mwisho.

VIJANA NA WATOTO WATAKIWA KUWA MACHO NA VVU NA UKIMWI

Na Godwin Msalichuma,
Mtwara,

VIJANA na watoto wametakiwa kuwa macho na ugonjwa wa UKIMWI kwani unaendelea kuuwa watu wengi miongoni mwa jamii yetu hii na kupunguza nguvu kazi katika kujitafutia maendeleo ya taifa letu ambapo asilimia kubwa ya idadi ya watu ni wao.

Rai hiyo ilitolewa na Afisa elimu Mkoa wa Mtwara Bw.Hipson Kipenya katika kongamano la Mtoto wa Afrika kimkoa lililofanyika hivi karibuni katika chuo cha ualimu ufundi Mkoani hapa ni katika kuadhimisha siku hiyo kimataifa.

Kongamano hilo liliandaliwa na asasi isiyokuwa ya kiserikali ya CYODO TANZANIA kwa ajili ya vijana na watoto wa Mikoa ya Mtwara na Lindi, ikiwashirikisha watoto na vijana kutoka katika shule za Msingi na Sekondari zilizotoa wawakilishi wawili wawili.

Bw.Kipenya alisema miongoni mwa mambo ambayo anatakiwa kuwakumbusha watoto na vijana kila akikutana nao ni juu ya ugonjwa huu hatari wa UKIMWI ambapo hakuwa na budi kuwasisitiza katika maadhimisho ya mtoto wa Afrika Kupitia Kongamano hilo.

“ Kabla sijafunga rasmi shughuli hii, napenda kuwakumbusha watoto na vijana kuwa ugonjwa wa UKIMWI bado unaendelea kuuwa watu wengi hapa Tanzania na Mkoani kwetu Mtwara……..na maambukizi bado yanaendelea kwa kasi….ninawaomba mjihadhari na tabia potofu ili muweze kujenga familia zenu na maisha bora siku zote za maisha yenu”alisema Bw.Kipenya.

Aidha aliwapongeza CYODO TANZANIA kwa jitihada zao za kuwasaidia vijana na watoto katika kuwawezesha kutambua haki zao na masuala yanayowahusu katika jamii yetu, na kuthubutu kwao kunaonyesha njia kwa mashirika mengine yasiyokuwa ya kiserikali kuiga mfano wao katika masuala ya ustawi wa jamii yetu ya Tanzania.

Mwisho WASHIRIKI SEMINA YA MAFUNZO YA GHARAMA ZA UCHAGUZI WAASWA

Na Godwin Msalichuma,
Mtwara.

WASHIRIKI wa semina ya mafunzo ya usimamizi na uelimishaji umma kuhusu sheria ya gharama za uchaguzi kutoka Mikoa ya Mtwara na Lindi, wameaswa kuzingatia mafunzo ya sheria hiyo na kanuni zake pindi watakapokuwa katika uelimishaji jamii, ili iweze kutofautisha uongozi wa kununuliwa na wa kuchaguliwa kwa ridhaa ya wananchi bila ya mgombea kutoa chochote.

Kauli hiyo ilitolewa hivi karibuni na katibu tawala msaidizi wa Mkoa wa Mtwara, Bw. Hemed Matuwira, alipokuwa anafungua mafunzo ya siku mbili juu ya wasimamizi wa uelimishaji umma kuhusu sheria ya gharama za uchaguzi wa mwaka huu yaliyofanyika katika ukumbi wa VETA Mtwara.

Bw.Matuwira ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa katika ufunguzi wa mafunzo hayo yanayoendeshwa na Taasisi ya elimu ya watu wazima , ambayo wameyapanga kikanda na kanda hii ni Mikoa ya Mtwara na Lindi ambapo washiriki 28 watahitimu, alisema kuwa washiriki hao wanapaswa kuielewa vizuri sheria hii ili watakapokuwa katika uelimishaji jamii iweze kutambua na kumhoji mgombea kuwajulisha gharama zake za uchaguzi amezitoa wapi.

“katika hili nataka mzingatie elimu mnayoipata leo ndiyo itakayowawezesha wagombea kuondoa dhana ya kununua kura za wananchi kwani watakuwa wameelimishwa vya kutosha na kutambua majukumu yao katika kuomba kura kwao badala ya kuwadanganya kwa kuwapatia fedha na vitu vingine…lakini kama kutatokea mgombea amekiuka hili basi ndipo sheria hii inapofanya kazi yake mara moja nasi tutaanza na huyo ili kutoa somo kwawengine ..maana huyo atakuwa ameshindwa kufuata kanuni na taratibu za sheria hii.” Alisema Bw.Matuwira.

Alisema kuwa elimu hii itasaidia wananchi kupata viongozi kwa taratibu zinazokubalika kisheria kuliko kutumiwa tu kama vyombo kwa kunuliwa kwa kuwa mgombea anafedha zake bila kujua kama niza halali ama la.

“Washiriki wote hapa mmetoka katika idara za elimu kwani tumetambua kuwa mnaweza kutoa mafunzo haya kwa wananchi kwa mafanikio makubwa kwani mnauelewa mkubwa katika ufundishaji…..wananchi wanapaswa kujua ni fedha kiasi gani zimetengwa kwa ajili ya chama Fulani na mgombea husika…hayo yote mnategewa nyinyi kuyafikisha huko.”alisema Bw.Matuwira.

Awali Msajili msaidizi wa vyama vya siasa Bw. Ibrahimu Mkwawa, alisema kuwa pindi kunapokuwa na malalamiko ya wananchi juu ya gharama za uchaguzi kutoka kwa mgombea au chama Fulani, kinachotumika ni ibara ya 24 ya sheria hii ambapo chama kitaombwa kubadili mgombea na kama hakitafanya hivyo msajili atakiwekea pangamizi kisiendelee na mchakato wa uchaguzi.

“Kama itatokea malalamiko ya wananchi kuwa na mashaka na gharama za mgombea wa chama Fulani, kuna ibara ya 24 ya sheria hii inamruhu msajili kuomba chama kubadili jina la mgombea anayelalamikiwa na kama chama hakitatekeleza hayo msajili anauwezo wa kuweka pingamizi kwa chama husika kwa mujibu wa ibara hiyo” Alisema Bw.Mkwawa.

Bw.Mkwawa alisema tayari wameshafikishiwa malalamiko katka ofisi ya msajili wa vyama vya siasa lakini hakuweza kubainisha ni mangapi na yanahusu vyama vipi vya siasa katika kinyang’anyiro cha uchaguzi wa mwaka huu.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment

Any