My Blog List

Sunday, July 8, 2012

WAKULIMA KUSINI WAGEUKIE UFUTA UNALIPA KULIKO KOROSHO

Na Godwin Msalichuma,
Mtwara,
CAR64FBH_0UKILIONA shina lake unaweza ukashangaa sana kwani kwa mbali unaonekani kama mmea mmoja hatari na haramu, mara ya kwanza nilijiuliza nilipokutana na shamba kubwa la maonyesho kwa wakulima ambalo lipo katika kituo cha utafiti wa kilimo na mifugo cha Naliendele Mtwara kilichopo kama kilometa 15 kutoka mjini. 

Kilichonishangaza katika mmea huo ni kwamba kuona kuwa unafanana kwa mwonekano haswa ukiwa mbali kidogo kama mimi nilivyokuwa ndani ya gari nikaona kama bangi ikanishangaza pia kulimwa tena karibu na barabara iendayo Tandahimba hadi Newala karibu kabisa na kituo hicho kikubwa cha utafiti katika Afrika.

Kabla sijauliza nilijiuliza mwenyewe moyoni kuwa ina maana kuwa katika kituo hiki cha utafiti wa kilimo wanatafiti pia zao la bangi? nikasema hapana itanibidi niulize wenyeji nilionao katika gari hili ninayoyaona ni kweli au naota ndoto za mchana.

Lakini kuna usemi unaosema kuwa anayeuliza anataka kujifunza ukanipa matumaini ya kuuliza ndipo nilipochukua uamuzi wa kufanya hivyo, nikamgusa jirani yangu tuliyekaa naye kiti kimoja “samahani kaka huku kwenu bangi zinaruhusiwa kulimwa”? Yule bwana alishituka kidogo na kunijibu kuwa hapana haziruhusiwi!.

Nikamwuliza tena kuwa sasa zile ninazoziona pale siyo bangi au macho yangu mabovu? Alicheka kidogo kabla hajanijibu kwa mara ya pili na kusababisha abiria wengine katika gari lile kukaa kimya na kutugeukia.Nadhani wengi huenda walisikia swali langu na wakataka kujua kuwa yule niliyemwuliza atajibu nini na pengine wengine wakafikiria huenda mimi siyo Mtanzania ndiyo maana nauliza swali kama lile.

Lakini bwana yule hakusita ndipo aliponijibu huku kukiwa na ukimya katika gari lile nadhani ni ukweli kwamba kila mmoja alitaka kujua kuwa nini kiliulizwa, akiwa na tabasamu akanijibu na kusema kaka zile siyo bangi ila ni zao la biashara huku kwetu kusini la ufuta. Ilikuwa ni kipindi cha masika nikiwa safarini kwenda Tandahimba kwa mara ya kwanza kwani nilikuwa mgeni bado Mkoani Mtwara nikitokea Dar es salaam. 

Ama kweli kutokujua ni kama usiku wa kiza ufuta ninaufahamu lakini shina lake nilikuwa sijawahi kuliona ndiyo kwanza hivi leo, lakini bado haliondoi ukweli wa kufanana na mmea wa bangi haswa ukiutazama kwa mbali kama ilivyokuwa kwangu nikiwa ndani ya gari. 

Hivi karibuni nilifanya ziara ya kutembelea kituo hicho cha utafiti na safari yangu kituoni hapo nilitaka kwenda kufuatilia zao la muhogo kama linaweza kuwa zao la kutegemea kwa kuokoa jamii kwa chakula.

Baada ya kuliona shamba lile ambalo bado halijaandaliwa kwa kilimo kwa sasa, ikabidi nibadili kibao pale pale baada ya kukumbuka kituko kile cha siku nasafiri kwenda Tandahimba nilipo ufananisha mmea wa ufuta na bangi nikajiambia itabidi nianze na zao hilo la ufuta kwanza. 

Nilianza safari yangu asubuhi kutoka Mtwara mjini kuelekea kituoni hapo baada ya kukaribia kituo hicho cha utafiti nilishitushwa na sauti ya konda ikisema risechi wapo? maana yake ni kituo cha utafiti kwa hiyo wao wanafupisha kwa kuita hivyo tena kwa Kiswanglishi? Nikaitikia kwa nguvu kidogo tupo shusha kitendo kilichofanya abiria wengine kunigeukia na kunikodolea macho. 

Ni sehemu iliyotambalale lakini imesongwa na vichaka vya miti ya asili kiasi kwamba huweza kuyaona majengo ukiwa mbali hadi ufike usawa kituo kilipo na katika mlango wa kuingilia kuna bango kubwa la mbao lililoandikwa Kituo cha utafiti wa kilimo na mifugo Naliendele Mtwara.

Nikaingia getini na kukutana na wazee wawili ambao nilihisi kabisa ndiyo wanaoshughulika na masuala ya ulinzi mlangoni hapo lakini pia wanatumika kama wapokeaji wa kuwaelekeza wageni kwenda sehemu ambayo ndiyo mahususi kwa mapokezi ya wageni na kuwakaribisha kwa kuwaelekeza kama wenyeji wao kituoni hapo wapo kazini au la.

Kama ilivyoada na mimi pia nikaelekezwa kwenda mapokezi nilikutana na mtu wa hapo ambapo nikamweleza kama naweza kuonana na mwenyeji wangu ambaye anahusika na zao la biashara la ufuta.

Ndipo nilipoambiwa yupo na ni Dkt.Omari Mponda ambaye ni mtafiti wa mbegu bora za mafuta kituoni hapo, ambapo lengo likiwa niweze kuzungumza naye kuhusiana na mmea ule niliouona kipindi hicho nasafiri na kuufananisha na mmea hatari wa bangi maana baada ya kudadisi pale mapokezi nikaambiwa yeye ndiye muhusika wa zao hilo.
Kijana wa mapokeza akaniambia nimfuate basi nikafanya hivyo ambapo akanipeleka katika jengo moja dogo jipya ambalo lilionyesha kuwa ndiyo kwanza linaanza kutumika baada ya kumalizika. 

Nilipokelewa vizuri na Dkt.Mponda ambaye kichwa chake kinapendeza kwa kuwa na mvi nyingi zilizoota bila kuacha madoa meusi kiasi kwamba unaweza kufikiri amemwagiwa unga kichwani ambapo zikionyesha kuwa ameshaukula chumvi nyingi kidogo, lakini kinachomsaidia ni kuwa mcheshi na anaonekana mwongeaji na mwenye kujiamini akiwa katika anga zake za kazi na kumficha hali yake hiyo ya uzee.

Karibu kijana Mimi naitwa Dkt.Mponda mtafiti wa mbegu bora za mafuta kituoni hapa. Asante mzee Mimi naitwa Bw.Godwin Msalichuma ni mwandishi wa habari nimekuja tuzungumze kuhusiana na zao la ufuta kwa ujumla katika kumwendeleza mwananchi wa kusini kiuchumi kwani nimeambiwa hapo nje kuwa ni zao la biashara kwa upande wa ukanda huu wa kusini.

Dkt.Mponda alianza kwa kutoa historia kidogo ya kituo cha utafiti Naliendele kwa kusema kuwa shughuli za tafiti za kilimo zilianza wakati wa ukoloni ambapo waliweka kituo Wilaya ya Nachingwea Mkoani Lindi na baada ya uhuru zilihamishiwa Ilonga Morogoro na hatimaye Mtwara mwaka 1978, ambapo mwaka 1983 tulikuwa na mbegu bora aina sita ambazo tulikuwa tumezifanyia utafiti na kushauri wakulima waweze kuzitumia mashambani.

Mwaka 1992 tulitafiti na kupata mbegu bora ya ufuta tuliyoipa jina la Naliendele 92 ambayo inazaa vizuri zaidi ya mbegu za awali, tukaendelea na tafiti ambapo mwaka 1994 tulikuwa na mbegu za aina mbili yaani zawadi 94 na Ziada 94 hizi tuliziingiza kwa ajili ya kuuza nchi za nje zaidi kuliko matumizi ya hapa nchini.

Tukaendelea na tafiti ambapo mwaka 2002 tukaingiza mbegu inayoitwa Lindi 2002 ambayo mpaka sasa inatumiwa na wakulima, sifa zake ni kwamba inavumilia sana magonjwa, ina vikonyo virefu ambavyo vina mifuko ya kubebea mbegu sita badala ya mbegu zingine kuwa na mifuko ya kubebea mbegu minne tu. 

Mbegu hii ilionekana kupendwa sana kwani tulipata maombi kutoka hata Mikoa ya Rukwa maeneo ya Mpanda na Mbeya katika maeneo ya Chunya na huku bado inaendelea kufanya vizuri katika kumwendeleza mwananchi kiuchumi.

Mwaka jana tukaingiza mbegu nyingine iitwayo Mtwara 2009 ambayo sifa zake ni kwamba inatoa mafuta mengi na kiurahisi sana wakati wa kukamua kwa kutumia LAM PRESS mashine ndogo za kusukuma kwa mkono ambazo tunashauri wakulima wadogo wadogo vijijini kutumia.

Anasema kuwa ndiyo maana tunawashuri wajasiriamali wa kati na wadogo kujiingiza katika kuyaongezea thamani kabla ya kuuza nje yakiwa ghafi haswa kukamua aina hii ya mbegu kwani ina mafuta mengi na ni rahisi kukamua.

Wajasiriamali wakigeukia zao hili linaweza kuwapatia kipato kwa haraka kuliko kung’ang’ania zao la korosho ambalo gharama zake za uzalishaji ni kubwa na bei yake ni ndogo ukilinganisha na ufuta ambao kilo moja kwa sasa inifika mpaka sh.1, 200 na ukisindika mafuta yanauzwa mpaka sh.5,000 kwa lita moja.

Dkt. Mponda anasema kuwa soko la ufuta ni kubwa sana na linahitaji kiwango cha tani nyingi kuweza kulitoshereza hivyo kujikuta kuwa ufuta unaweza ukatoa ajira kwa wananchi wengi zaidi katika kulima na hata katika kusindika mafuta ili kuliongezea thamani kabla ya kuuza katika soko la nje.

“Ninashauri wajasiriamali kujiingiza katika kulima na kusindika ufuta kwani wataweza kupata faida kubwa kwa muda mfupi zaidi kuliko kukimbilia mazao mengine kwa mazoea tu kama korosho lakini mwisho wa siku hayana tija kama lilivyo hili zao” alisema na kuongeza. 

“Unaposindika ufuta hata mabaki yake ni biashara kwenye upande wa mifugo, kwahiyo unakuta mafuta unauza na mabaki unayauza pia….na kwa mkulima unaweza kuanzisha ufugaji wako mwenyewe hivyo kuboresha maisha yako  ”. Alisema mtafiti huyo. 

Alisema kuwa ufuta una wadudu ambao huwa wanasumbua na kushaumbulia wakati ukiwa shambani lakini ukifuata ushauri wa kutumia mbegu bora na kanuni za ukulima wa kisasa na kupata madawa ya kupulizia katika hekta moja unaweza kuvuna tani 1.5  ambapo hicho ni kiwango kizuri cha mapato.

Anatoa ushauri kuwa kabla hawajajiingiza katika kilimo hiki cha ufuta wanaombwa kuja kuwaona watafiti ili kuweza kupata mahitaji ya kitalaamu ya uzalishaji wa zao hilo na pia kupata historia ya ukulima bora kutoka kwa wakulima wengine kwani vyote vinapatikana hapo kituoni.

Hakusita kuificha furaha yake ya kutembelewa na mwandishi wa habari kituoni hapo kwani aliona kuwa na mwanahabari pale ni njia mojawapo ya matokeo yao ya tafiti yanaweza kuwafikia wananchi waliowengi zaidi hivyo kumkaribisha tena kuja kupata matokea mbalimbali ya tafiti zinazokuja.

Mwandishi wa makala haya alijaribu kumwuliza kuhusu jamii inayozunguka kituo hicho inanufaika vipi na tafiti mbalimbali ambazo zinafanyika kituoni hapo, naye alisema zaidi ya kunufaika na kazi za vibarua zinazopatikana pale huwa hawajisumbui katika masuala mazima ya ukulima kwani ni kwa uchache sana katika mazao ya muhogo na korosho ndiyo wanayojishughulisha nayo.

“Wengi wanaotuzunguka hapa wanaridhika na vibarua wanavyopata hapa hivyo hawajisumbui kabisa katika ukulima wa mazao haya tunayoyafanyia tafiti hapa…kwahiyo waandishi mtakapowaelimisha wanaweza kubadilika na kutambua faida ya kuwa karibu na kituo cha utafiti” alisema Dkt.Mponda.

Mbali na kufanya tafiti za mbegu bora lakini pia wanatoa ushauri wa masoko na panapolazimika huwatafutia wakulima wanaozalisha mbegu bora kupata sehemu za kuuzia mazao yao hayo kwani pia kituo kinatoa mafunzo kwa wakulima kuzalisha mbegu bora ili kuwauzia wenzao kipindi cha msimu wa mvua.

Jukumu hili la kuwaelimisha wananchi watafiti wanashauri lisiachiwe wanahabari na vyombo vyao bali pia hata halmashauri zinatakiwa kuandaa mipango ya kuwaelimisha wananchi kuchangamkia matokeo ya tafiti mbalimbali za kilimo.

Kwani halmashauri nyingi hapa nchini zinanufaika na ushuru wa mazao yanayolimwa katika maeneo yao hivyo wanaombwa kusaidia katika msukumo ili wanapowakata wakulima basi nao wawe wamechangia katika mapato hayo yanayoendeleza taifa letu kimiundombinu.